Michezo yote 10 ya wiki ya saba ya EPL imeshachezwa. Kwenye
makala hii mwandishi wetu amechagua kikosi cha wachezaji 11 waliofanya
vizuri kwenye michezo ya EPL wiki hii.
Golikipa: HUGO LLORIS (Tottenham)
Alitoa mchango wa kutosha dhidi ya Man City. Aliokoa
michomo ya hatari kutoka kwa Kolarov, Sterling na Jesus Navas kwenye
vipindi vyote viwili kwenye mchezo huo ambapo timu yake iliibuka na
ushindi wa mabao manne kwa moja.
Mlinzi wa Kulia: DARYL JANMAAT (Newcastle)
Alimdhibiti Eden Hazard kwa kiasi kikubwa na alipandisha
vizuri mashambulizi ya Newcastle hapo juzi hasa kwenye kipindi cha
kwanza. Kutokana na kujaribu kulinda mabao ya timu yake kipindi cha pili
alilazimika kupunguza mashambulizi.
Mlinzi wa Kati: BREDE HANGELAND (Crystal Palace)
Aliiwezesha Crystal Palace kumaliza mchezo wa juzi bila
kuruhusu bao dhidi ya Watford. Hilo liliwezekana kutokana na mlinzi huyo
kuwazima washambuliaji wa Watford wakiongozwa na Ighalo kila
walipojaribu kuleta madhara.
Mlinzi wa Kati: VIRGIL VAN DIJK (Southampton)
Ingawa Swansea walipiga mashuti 11 kwenye mchezo wa juzi
lakini mengi kati ya hayo yalipigwa na viungo nje ya eneo la hatari.
Washambuliaji wa Swansea walidhibitiwa vyema na van Dijk na hawakuweza
kudhuru ngome.
Mlinzi wa Kushoto: MATTEO DARMIAN (Manchester United)
Kwenye mchezo dhidi ya Sunderland hapo juzi Darmian
aliliziba vema pengo la majeruhi Luke Shaw. Kiwango alichoonyesha kwenye
mchezo huo kinatosha kabisa kumfanya van Gaal aendelee kumtumia kama
mbadala wa Shaw.
Kiungo wa Kati: ERIC DIER (Tottenham)
Siri ya mafanikio ya Tottenham kwenye mchezo wa hapo juzi
dhidi ya Manchester City ilikuwa namna Dier alivyowazima viungo wa
Manchester City dakika zote za mchezo. Ushindi wao wa 4-1 ulichangiwa
mno na kiwango cha Dier.
Kiungo wa Kati: JAMES MILNER (Liverpool)
Ukiacha bao la kuongoza aliloifungia Liverpool dhidi ya
Aston Villa hapo juzi Milner alionyesha kiwango kikubwa kwenye mchezo
huo. Alikuwepo kila mahala alipohitajika na akatekeleza vyema majukumu
yake uwanjani.
Kiungo wa Kulia: ERIK LAMELA (Tottenham)
Winga huyu aliwapa tabu mno walinzi wa Manchester City
kwenye mchezo wa juzi. Kiwango alichokionyesha kilitosha kabisa kumfanya
ang’are kwenye mchezo huo baada ya kutengeneza bao moja na kufunga
lingine zuri.
Kiungo wa Kushoto: ALEXIS SANCHEZ (Arsenal)
Huyu hahitaji maelezo mengi. Hat-trick aliyoifungia Arsenal
kwenye mchezo wa hapo juzi dhidi ya Leicester City imemfanya kuweka
rekodi ya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga hat-trick kwenye ligi zote
tatu za Italia, Hispania na England.
Mshambuliaji: DANIEL STURRIDGE (Liverpool)
Majeraha yalimuweka nje kwa miezi mitano lakini hapo juzi
kwenye mchezo dhidi ya Aston Villa mshambuliaji huyu alionyesha kuwa
hahitaji muda mrefu kurudi kwenye ubora wake. Aliwasumbua walinzi na
akaifungia timu yake mabao mawili.
Mshambuliaji: ROMELU LUKAKU (Everton)
Lukaku alimalizia vizuri nafasi alizopata kwenye mchezo wa
jana dhidi ya West Bromwich na kufunga mabao mawili likiwemo bao la
ushindi alilofunga kwenye dakika ya 84. Zaidi ya hapo Lukaku alitoa pasi
ya bao la Arouna Kone.


Post a Comment