Kocha Mkuu wa Yanga George Lwandamina, amesema timu yake itafika mbali kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutokana na udhaifu wa timu alizopangiwa nazo hadi kufikia hatua ya makundi.
Shirikisho la Soka Afrika (CAF), wiki hii lilitoa ratiba ya michuano ya Ligi ya Mabingwa na ile ya Kombe la Shirikisho, ambapo Yanga imepangwa kuanza hatua ya awali Ligi ya Mabingwa Afrika na timu ya Ngaya de Mbe ya Comoro.
Lwandamina, alisema anatambua soka la Afrika limebadilika sana, lakini anajivunia ubora wa timu aliyo nayo, ambayo inafanana na ukubwa wa mashindano wanayoenda kuyakabili.
“Nafahamu hii ni michuano mikubwa Afrika, lakini lengo letu Yanga ni kucheza fainali na kuwa mabingwa. “Tumepangiwa kuanza Comoro najua taifa hilo nidhaifu bado lipo nyuma kisoka, lakini hatutowadharau tutacheza kwa nguvu na kuhakikisha tunafuzu kwa kishindo,” alisema Lwandamina.
Mzambia huyo alisema kutoka mapema kwa ratiba hiyo kumemsaidia kuwajua wapinzani wao na kuanzia sasa atabadili programu ya mazoezi ili kuhakikisha wanakuwa bora zaidi ya ilivyo sasa. Alisema kwa kua hawatakuwa na muda wa kutosha kujiandaa na michuano hiyo atazitumia mechi za Ligi Kuu kama vipimo kuelekea kwenye michuano hiyo.
“Ratiba ya ligi inaonekana kubana, ni wazi hatutokuwa na muda kufanya maandalizi maalumu kwa ajili ya michuano ya Caf, ispokuwa nitabadilisha program ya mazoezi kwa kuongezea vitu vingine vya msingi na kutumia mechi za ligi kama majaribio,” alisema.
Kwa mujibu wa ratiba ya Caf, Yanga itaanzia ugenini Comoro mechi ya kwanza ikichezwa kati ya Februari 10 hadi 12 na ile ya marudiano ikipangwa kuchezwa Uwanja wa Taifa Dar es Salaam kati ya Februari 17 hadi 19 na ikifuzu itakutana kati ya Zanaco ya Zambia au APR ya Rwanda.
Post a Comment