Na Samuel Samuel
Wakati Simba SC wakiiweka rehani leseni ya beki wa kulia wa Young Africans Hassani Kessy kuichezea timu hiyo kwa kile kinachodaiwa mchezaji huyo na klabu ya Young Africans kukiuka mkataba wa awali wa klabu hiyo na mchezaji huyo , Simba imeuvagaa mkenge kwa mchezaji wao wakimataifa Laudit Mavugo waliyemsajili siku nne zilizopita kwa kandarasi ya miaka miwili.
Klabu ya Vitalo 'O inayoshiriki ligi kuu nchini Burundi imetanabaisha bado ina mkataba wa mwaka mmoja na mshambuliaji huyo tegemeo kwenye timu hiyo na imeshitushwa sana kusikia na kuona Mavugo katia Tanzania kwenye klabu ya Simba bila ya wao kuwa na taarifa.
Vitalo 'O wamesisitiza jina la mshambuliaji huyo lipo kwenye orodha yao iliyoenda CAF na ndani ya shirikisho la soka nchini Burundi kwa msimu ujao wa ligi.
Tayari klabu hiyo imeamua kuishitaki Simba SC FIFA kuingia mkataba na mchezaji wao aliye ndani ya kandarasi ya mwaka mmoja muda ambao unamzuia mchezaji kufanya mazungumzo na klabu yoyote kiusajili bila klabu husika kupitia kwa timu stahiki yenye kandarasi na mchezaji juu ya miezi sita.
Vitalo ' O wanasisitiza kufanyiwa hujuma na wakala wa mchezaji wao na viongozi wa Simba SC baada ya mchezaji huyo kuomba kibali cha kwenda ufaransa kwenye majaribio ya kuichezea timu moja ya second division lakini ghafla wanashangaa mchezaji huyo kutua Tanzania kwa klabu ambayo wamekuwa wanashindwana kufikia muafaka kwa muda mrefu kuhusu manunuzi ya mshambuliaji huyo.
Simba SC bado wapo kimya kujibu tuhuma hizo lakini kama ni kweli mchezaji huyo ana kandarasi ya mwaka mmoja na Vitalo 'O na tayari wamemvisha jezi za timu hiyo na kuichezea klabu hiyo mechi ya kimataifa dhidi ya AFC Leopards toka Kenya, basi Simba SC wanakila dalili kukumbana na rungu la FIFA.
Nini kinaendelea Tanzania ?! Kila kukicha ni vituko ndani ya soka la nchi hii kuanzia ngazi ya shirikisho jadi kwenye vilabu.
Nachelea kuamini klabu kongwe kama Simba SC kufanya uhuni huu ilihali taratibu wanazijua . Tusubiri tamko la klabu hiyo maana haingii akilini Simba SC kumsajili mchezaji wakimataifa bila kujua kandarasi yake na timu ya awali .ITC yake wataipata vipi, ?
Huenda Vitalo 'O wanakurupuka kuibania Simba SC ? Muda utaongea
Wanyetishaji ndani ya Simba SC wanadai kumsajili mchezaji huyo akiwa huru na Vitalo ' O wanaleta kauzibe kutaka faranga toka Simba SC . Nani mkweli ?! muda ni hakimu wa haki.
Post a Comment