Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara
msimu wa 2016/17 inatarajiwa kuanza kesho Jumamosi Agosti 20, 2016 kwa michezo
mitano huku Bingwa Mtetezi wa Kombe hilo 2015/16, Young Africans ya Dar es
Salaam ikisubiri hadi Agosti 31, 2016 kuanza kutetea taji lake.
Young Africans inatarajiwa kusafiri
kwenda Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), kucheza na TP Mazembe kwenye
mchezo wa Kombe la Shirikisho unaotarajiwa kufanyika Agosti 23, mwaka huu.
Michezo itakayochezwa kesho ni
pamoja na Simba SC itakayoikaribisha Ndanda FC ya Mtwara kwenye Uwanja wa
Taifa, ulioko Chang’ombe Dar es Salaam, katika mchezo utakaoanza saa 10.00
jioni wakati Azam itakuwa mwenyeji wa African Lyon kwenye Uwanja wa Azam FC
ulioko Chamazi-Mbagala, nje kidogo ya jiji.
Kadhalika Stand United ya Shinyanga
itakuwa mwenyeji wa Mbao FC ya Mwanza kwenye Uwanja wa CCM Kambarage mkoani
Shinyanga sawa na Mtibwa Sugar itakayoikaribisha Ruvu Shooting ya Pwani kwenye
Uwanja wa Manungu uliuoko Turiani, Mvomero mkoani Morogoro wakati Prisons ya
Mbeya itasafiri hadi Uwanja wa Majimaji ya Songea kucheza na Majimaji FC ya
huko.
Wakati ligi ikianza, Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) linaonya timu kuchezesha wachezaji wa kigeni kama
hawana vibali vya kuishi, kufanya kazi na leseni inayomruhusu kucheza ligi
husika kwa mujibu wa sheria za nchi na kanuni za Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania
Bara.
Vibali vya kuishi na kufanya kazi
vinatolewa na Idara ya Uhamiaji Tanzania (Uhamiaji) wakati leseni ya kucheza
inatolewa na TFF. Vilevile tumeziagiza klabu kulipia ada za ushiriki kwa kila
timu; leseni za wachezaji, ada za wachezaji na ada za mikataba. Mchezaji
hatapewa leseni ya kucheza kama uongozi wa timu hautakamilisha taratibu za
malipo.
TFF inapenda kuzikumbusha timu
zinazoshiriki Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania Bara kwamba hatutatoa leseni ya
mchezaji yeyote ambaye timu haikuleta mkataba wakati wa maombi ya usajili, hii
ni kwa mujibu wa kanuni ya 68 vipengele vya 1, 2, 3 na 8 ya Ligi Kuu ya
Tanzania toleo la 2016/2017.
Kila timu inatakiwa kuleta nakala
tatu za mkataba wa mchezaji, ili kamati ya katiba, sheria na hadhi za wachezaji
iweze kupitia na TFF iweze kuidhinisha mikataba hiyo. Baada ya hapo timu na
mchezaji, watakuja kuchukulia mikataba hiyo hapa TFF. Ni matarajio yetu kuwa
kila klabu itatimiza wajibu wake ili kuondoa migogoro kati ya timu na mchezaji
na mchezaji na timu. Tunategemea kupata ushirikiano.
Post a Comment