AMEKUBALI! Ndivyo unavyoweza kusema kutokana na kauli ya Kocha Jose Mourinho, ambaye amemmwagia sifa kinda wake, Marcus Rashford.
Wakiwa ugenini dhidi ya Hully City ya Kocha Mike Phelan, Manchester United walipata ushindi mwembamba wa bao 1-0 dhidi ya wapinzani wao hao.
Alikuwa ni kinda huyo Mwingereza aliyewainua kwenye viti mashabiki wa Man United kwa kuandika bao hilo katika dakika ya 92 ya mchezo huo wa Ligi Kuu England.
Man United waliingia uwanjani wakiwa na kiu ya kuendeleza ushindi katika ligi mara baada ya kushinda michezo yao miwili ya mwanzo.
Huenda mchezo huo ungekwisha kwa matokeo ya kutofungana, lakini Rashford aliitumia vyema pasi ya nahodha wake, Wayne Rooney.
Kwa kufunga bao hilo, chipukizi huyo ameiwezesha Man United kuendeleza rekodi yao ya ushindi waliyoianza katika mchezo wa kwanza wa Ngao ya Hisani, ambapo waliibuka na ushindi mbele ya mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya England, Leicester City.
Hata hivyo, Mourinho amekuwa akimtegemea zaidi straika wake mpya raia wa Sweden, Zlatan Ibrahimovic, aliyetoka kwa matajiri wa Jiji la Paris, PSG.
Mpaka sasa staa huyo ameshaifungia klabu hiyo mabao matatu tangu aliposajiliwa.
Rashford ataendelea kubaki vichwani mwa mashabiki wa Arsenal, kwani ndiye aliyetia ‘gundu’ safari yao ya kuchukua taji la ligi.
Baada ya kufungwa mabao 3-1, huku Rashford akitupia mawili, Gunners walianza kupokea vipigo mfululizo na hatimaye kupotea kwenye mbio za ubingwa.
Mshambuliaji huyo tayari ameitwa mara kadhaa kuiwakilisha timu ya Taifa ya England, licha ya kikosi hicho kuwa na mastaa kama Jamie Vardy na Harry Kane.
Nyota ya Rashford ilianza kung’aa wakati wa utawala wa Mholanzi Louis van Gaal.
Mara baada ya Mholanzi huyo kufungashiwa virago vyake klabuni hapo, ziliibuka tetesi kuwa huenda safari ingemkuta nyota huyo.
Itakumbukwa kuwa makinda wenzake kama Donald Love, Paddy Mc Nair tayari wameshatimka klabuni hapo na kujiunga na Sunderland.
Kinyume na matarajio ya wengi, Rashford ameonekana kuendana na kasi ya mafanikio ya Mourinho ambaye tayari ameahidi kuipa Man United ubingwa katika msimu wake wa kwanza.
“Marcus (Rashford) ni mchezaji mzuri, mwenye uwezo mkubwa wa kufunga na kutoa pasi za mwisho. Huwezi kuamini, ndiye aliyeamua matokeo yetu katika mchezo huu wa leo uliokuwa mgumu kwetu tulipokuwa ugenini.
Alisema kuwa kinda huyo ni mbadala sahihi wa mshambuliaji mkongwe wa klabu hiyo, Zlatan Ibrahimovic, ambaye ni mshambuliaji wao namba moja ambaye anafanya vizuri, licha ya ugeni katika Ligi Kuu England.
“Marcus (Rashford) ni mshambuliaji kinda lakini uwezo wake bado haujakaa sawa, ndiyo maana tulimnunua mshambuliaji mwingine mkongwe ili tumpe uzoefu mchezaji huyu ambaye ameonyesha kuwa na kitu cha ziada.
“Zlatan ni bora, ni mchezaji mwenye kila kitu anachotakiwa kuwa nacho mshambuliaji wa kisasa, anacheza na kumuonyesha kinda huyo kuwa kuna mambo ya kujifunza kwa staa huyo mkongwe na Marcus ataendelea kuwa mshambuliaji namba mbili nyuma ya mkongwe huyu,” alisema.
“Ataendelea kupewa nafasi katika kikosi ili aendelee kupata uzoefu, ni moja kati ya vijana wenye kipaji cha hali ya juu sana katika kikosi cha Manchester, atakuwa hazina ya klabu siku za usoni,” alisema.
Kwa upande mwingine, Mourinho amesema kinda huyo hatapata nafasi ya kuanza katika kikosi cha kwanza na badala yake atakuwa akipewa muda mchache na si kucheza dakika zote 90.
Aliongeza kuwa Rashford atakuwa akipewa nafasi ya kumalizia mchezo ili kuendelea kutunza kiwango chake ambacho kitakuwa faida kwa klabu ya Man United na England.
Akiuzungumzia mchezo dhidi ya Hull City, Mourinho alisema ushindi wa ugenini dhidi ya wapinzani wao hao ulikuwa wa kuvutia kwa kikosi chake na pia walicheza kwa tahadhari kubwa.
About Author
The part time Blogger love to blog on various categories like Web Development, SEO Guide, Tips and Tricks, Android Stuff, etc including Linux Hacking Tricks and tips. A Blogger Template Designer; designed many popular themes.
Advertisement
Subscribe to:
Post Comments (Atom)


Post a Comment