Mashindano ligi ya vijana yamefunguliwa rasmi leo katika uwanja wa Kaitaba mkoani Kagera .
Mashindano hayo yanayoshirikisha vijana chini ya miaka 20 wanaunda timu za vijana za ligi kuu Tanzania bara , yamegawanywa katika makundi mawili moja likiwa mkoani Kagera na la pili jijini Dar es salaam.
Uwanja wa Kaitaba leo ambapo imefanyika mechi ya ufunguzi kati ya Yanga SC na wenyeji Kagera Sugar imeishia sare ya 1-1 vijana wa Kagera wakichomoa goli dakika za nyongeza kipindi cha pili.
Mchezo ulikuwa mkali na wa kuvutia timu zote zikishambuliana kwa zamu na kuonesha hali kubwa ya kuukamia ushindi.
Vijana wa Yanga SC wakiongozwa na kiungo mshambuliaji Yusufu Mhilu ambaye pia anachezea timu ya wakubwa, dakika 30 za awali walilishambulia sana lango la Kagera ambao walikuwa wakicheza kwa kujihami kukinzana na mashambulizi ya watoto hao wa Jangwani chini ya Shadrack Nsajigwa.
Baada ya kuwasoma vyema Yanga SC , Kagera walianza kuipeleka puta Yanga SC kwa mashambulizi makali ambayo yaliwafanya Yanga kurudi nyuma na kucheza kwa kujilinda na kutengeneza mashambulizi ya kushitukiza kupitia kwa Yusufu Mhilu na Samweli.
Timu zote zilikwenda mapumziko bila goli .
Kipindi cha pili kilianza kwa kasi na vijana wa Shadrack Nsajigwa wakitumia mfumo wa 4-4-2 waliweza kuichachafya ngome ya Kagera Sugar hali iliyowafanya wanankurukumbi hao kurudi nyuma na muda mwingi kucheza faulo.
Dakika ya 68 Yanga SC walipata faulo wing ya kushoto . Mpira huo wa adhabu ndogo ulichongwa vyema na beki wa kulia wa timu hiyo na kumfikia Yusufu Mhilu aliyeutia kambani kwa kichwa huru akiwazidi vyema walinzi wa Kagera Sugar.
Yanga wakiamini mchezo umekwisha kwa ushindi wa 1-0 , dakika ya 94 muda wa nyongeza Kagera Sugar walifanya shambulizi kali la kuvizia zikipigwa pasi mbili ndefu tu na Christopher Pascal kuutia nyavuni mpira . Goli ambalo liliwaumiza vijana hao wa Yanga SC.
Upande wa Yanga SC , Nsajigwa anahitajika kuisuka vyema safu yake ya mashambulizi hususani utulivu na umakini katika kushambulia kwani walikosa magoli mengi sana.
"kikosi changu kimekwazika sana na sare hii lakini tunajipanga kwa mchezo ujao na kwakweli huu ndio ulikuwa mchezo mgumu kwetu na pia uchovu nao umechangia kwa kiasi flani"alisema mwalimu Nsajigwa
Pia mwalimu aliongeza
"pia mpira unamatokeo matatu ni haya ya leo ni moja wapo ya matokeo pia kikubwa mashabiki wetu waendelee kutupa sapoti ya kutosha kwenye michezo inayofuata"


Post a Comment