Na Samuel Samuel
Ni mchezo mgumu kwa pande zote mbili ingawa mizani ya tathimini inaipa nafasi kubwa Simba SC kuibuka kidedea katika mchezo huu muhimu kwao kuendelea kujisafishia njia ya ubingwa msimu huu.
Katika mechi tatu za mwisho kabla ya mchezo wa leo, Ruvu Shooting imeonesha kuimarika na kuthubutu kutetea nafasi yao katika jedwali la ligi kuu msimu ujao.
17 Desemba ufunguzi wa duru la pili la ligi kuu, Ruvu Shooting walitoka sare ya 1-1 na Mtibwa Sugar ilihali wakati ligi inafungwa kwa kupisha mapumziko ya dirisha dogo la usajili, Ruvu walikubali kichapo cha goli 2-1 kwa Yanga SC. Mchezo wao wa mwsho kabla ya leo yaani 26 Desemba waliwachapa 2-0 Tanzania Prisons nyumbani.
Kimbinu na kiufundi utaona ni timu inayoimarika . Timu ambayo ipo nafasi ya sita! katika msimamo wa ligi ikiwa na alama 23 baada ya kucheza michezo 17 ikishinda mitano, sare nane na kufungwa michezo minne tu!.
Ni aina ya timu ambayo inacheza sana mchezo wa kujilinda na kushambulia kwa kushitukiza . Ni ngumu kuipita safu yao ya ulinzi na eneo la kiungo cha chini ingawa wana safu dhaifu ya ushambuliaji . Hili linaonekana kwenye idadi ya mechi walizotoka sare kuwa ni nusu ya mechi zote walizocheza mpaka sasa na theluthi moja ya mechi hizo wakishinda . Wameshinda mechi tano na kupoteza nne. Si timu ya kubeza kwenye ulinzi.
Simba SC wenye kiu ya ubingwa wanakutana na timu ambayo si mbaya kimbinu na kiufundi . Ni timu yenye msingi mzuri wa " team work " na kujua vyema kucheza na vigogo wa ligi.
Mechi ya mzunguko wa kwanza tarehe 7 Septemba, Simba walishinda 2-1 uwanja wa taifa jijini Dar. Magoli ya Simba yakifungwa na Ibrahimu Ajibu na Laudit Mavugo. Leo Simba wanakosa huduma ya Ajibu aliyeko Morocco kwa majaribio ya soka la kulipwa lakini ingizo jipya la Pastory toka Stand United ni mtihani kwa Shooting. Ana uwezo mkubwa kucheka na nyavu na kuwachezesha wenzake .
Matokeo ya Yanga jana ambayo yamewafanya kuwakaribia Simba kwa tofauti ya alama moja, ni mtihani mwingine kwa Ruvu Shooting. Simba wanaingia uwanjani wakiwa na mawazo ya kuzidi kutengeneza tofauti kubwa ya alama kati yao na Yanga .
Kama kawaida yao , Simba wanaingia uwanjani leo na mfumo wao wa 4-4-2 kwa aina ya kikosi kilichotoka .
Besala Bukungu na Zimbwe Jr wanatarajiwa kusaidia timu katika mashambulizi ya pembeni ingawa Omog si muumini sana wa kutumia walinzi wa pembeni kujenga mashambulizi kamili ya upande ila huwatumia kwenye " counter " tu hususani kushoto kwa Zimbwe Jr.
Mbinu kubwa za Omog kwenye mchezo huu ni safu yake ya kiungo. Amewapanga Jonasi Mkude kama kiungo mkabaji , kotei kulia kwake kama kiungo mkabaji wa ziada hii ina maana timu inaingia na 4-4-2 lakini kwa kutumia " double six ".
Mohamed Ibrahimu ameshushwa kucheza namba 8 kama kiungo huru , ikitarajiwa Mkude kutawala eneo lote kwa back up ya Kotei . Hii ina maana kuna wakati Simba wanategemea kubadilika kwa 4-3-3 wakiwa na viungo wengi mbele kumshambulia shooting.
Pastory atakuwa mwiba kwa Ruvu Shooting lakini akitegemea zaidi uwiano wake na MO Ibrahim kwenye " direct play " pia Shiza Kichuya aliyepangwa kushoto leo . Ni nafasi nzuri kwake kutokana na matumizi ya mguu wa kushoto pia uwezo wa kutengeneza krosi au kushambulia akitokea pembeni kama inside left.
Ni mechi ngumu na imepangwa kiufundi hivyo sote tutegemee burudani nzuri.
Asanteni.
Post a Comment