Sehemu ya makaburi ya wachezaji wa kikosi cha KK 11 waliofariki kwa ajali ya ndege katika fukwe za Gabon mwaka 1993.
Hiki ni kikosi cha timu ya taifa ya Zambia ambao kwa sasa wanajuliikana sana kwa jina la Chipolopolo yaani risasi za shaba.
Pichani ni msafara wa klabu ya Yanga SC ulivyozuru katika makaburi hayo na kupiga picha ya pamoja kwenye mnara wa kumbukumbu uliopo pembezoni tu mwa uwanja wa mashujaa jijini Lusaka . Uwanja uliojengwa na kutunza kumbukumbu hiyo muhimu kitaifa.
Mapenzi makubwa ya wazambia na Afrika kwa ujumla kwa wahanga hawa wa ajali hii mbaya katika taifa hilo , huwafanya watu wengi kuutazama uwanja wa mashujaa wa Lusaka kama sehemu ya huzuni licha ya uzuri wake.
Kuna wakati fulani Kalusha Bwalya alikaririwa na vyombi vya habari vya nchi hiyo akisema ; " ni nadra sana kuhudhuria kila tukio katika uwanja wa mashujaa. Mara nyingi nikiwa ndani ya uwanja huo machozi hunitoka nikikumbuka rafiki na ndugu zangu tuliokuwa kikosi kimoja " alieleza Bwalya kwa uchungu.
Bwalya hakuwepo kwenye kikosi hicho kilichopata ajali . Bwalya ambaye alikuwa nahodha wa timu hiyo alikuwa nchini Uholanzi na timu yake ya PSV na ilikuwa aungane na wenzake nchini Senegal baada ya mchezo huo.
Kikosi cha wachezaji 18 pamoja na kocha wao walipoteza maisha katika ajali hiyo mbaya na wafanyakazi wote wa ndege baada ya rubani wa ndege ya kijeshi Zambian Air Force de Havilland Canada DHC-5D Buffalo iliyokuwa na usajili namba AF-319 kuzima injini ambayo ilikuwa nzima akichanganya na mbovu iliyokuwa imeshika moto. Ajali hii mbaya ilitokea jioni ya tarehe 27 April 1993.
Ni ukweli usiopingika kikosi hiki kilikuwa moja ya vikosi bora Afrika kuanzia mwaka 1988 wakikumbukwa kwa ushindi wao wa 4-0 dhidi ya Italia jijini Seoul Korea Kusini kwenye michuano ya Olympic.
Yanga SC wanaingia katika orodha ya vikosi mbali mbali ngazi ya klabu na timu za taifa zilizopata kuzuru makaburi hayo.
Imeandikwa na Samuel Samuel


Post a Comment