Na Jeff Gemo
Majira ya saa kumi kamili jioni , jiji la Dar es salaam na viunga vyake watashuhudia miamba miwili ya soka nchini wana lamba lamba Azam FC wakipepetana na mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara Yanga SC katika mchezo wa raundi ya 25 ligi kuu.
Hivi karibuni vilabu hivi viwili vimekuwa na upinzani mkali hali inayoongeza joto la mchezo wa leo .
Toka Azam FC wapande ligi kuu msimu wa 2008-9, wamekutana mara 18 Katika michezo hiyo 18 Yanga wameshida mara 5 na Azam FC wameshida mara 5 na wakitoa Sare Mara 8 kila timu imemfunga mwenzake goli 25. Rekodi hii inakupa tathimini fupi ya ubabe uliopo kati ya timu hizi mbili . Mpaka sasa hakuna mbabe kati yao ambaye anaweza kutamba kifua mbele kumgaragaza mwenzake.
Hii inatupa picha kamili ya mechi ya jioni ya leo itakavyokuwa na upinzani mkali.
-Kimbinu na kiufundi
Tukianza na Azam FC mabingwa mara moja ligi kuu Tanzania bara msimu wa 2013-14, wanaingia uwanjani leo wakiwa na mtaji mzuri kisaikolojia baada ya kuitungua Yanga SC 4-1 kule Zanzibar katika mashindano ya kombe la Mapinduzi. Hali hii itawafanya kuikabili Yanga wakiwa na hali ya kujiamini na kutaka kuendeleza ubabe huo pia tension ya Yanga kutotaka kupoteza mechi mbili mfululizo inaweza kuwafanya kucheza mchezo wa kujilinda zaidi na kuwapa nafasi wao kuwashambulia muda mwingi .
Azam FC wanamkosa mshambuliaji wao na nahodha wa kikosi hicho John Bocco mwenye bahati ya mtende kuwatungua Yanga SC . Bocco peke yake katika goli 25 ambayo Azam FC kaifunga Yanga , magoli 13 yamefungwa na mshambuliaji huyo ambaye leo atakuwa mtazamaji kutokana na upasuaji wa mguu wake aliofanyiwa.
Hii haiwafanyi Azam kuwa na safu ya ushambuliaji butu dhidi ya Yanga leo. Silaha kubwa ya Azam ni safu yao ya kiungo cha kati na mawinga wa pembeni .
Kwenye mechi zote mbili za Taifa Stars dhidi ya Botswana na Burundi, Himidi Mao Mkami aliituliza vyema safu ya kiungo hali inayowapa uhakika benchi la ufundi la Azam FC chini ya mromania Cioaba kama watamwanzisha leo , kuitendea haki nafasi hiyo ikiwa ni consistency nzuri kimbinu.
Safu ya kiungo ya Yanga SC inatabirika na haijawa na mwendelezo chanya mpaka sasa licha ya ujio wa Justin Zulu lakini utawaona Mao Mkami , Frank Domayo na Abubakary Salumu wamekuwa na muunganiko mzuri na wote wana shabihana kiutendaji. Kiasilia wote ni box to box midfielder hivyo Lwandamina kama hajajipanga vyema katika safu hii leo atagemee upinzani mkali kama ule wa Mapinduzi.
Ukiondoa mechi ya Lesotho waliyopoteza 3-0 , rudi kwenye mechi ya awali jijini Dar es salaam wakicheza na Mbabane Swallows. Azam FC ambao wapo katika kipindi cha mpito wakijifunza mbinu mpya za benchi lao la ufundi , wamekuwa na uwezo mzuri kumiliki mpira , kujilinda na kushambulia pande zote ingawa bado wana tatizo dogo la kushindwa kuzitumia nafasi wanazotengeneza.
Kukosekana kwa Bocco leo , ina maana Yahya Mohamedi anaweza kuanza kama mshambuliaji kiongozi katika mfumo wao wanaotumia sana wa 4-3-3 . Kushoto akizungukwa na Joseph Mahundi na kulia Ramadhani Singano . Chini yao wakisimama Himidi Mao , Domayo na Sure Boy . Hii inaweza kuwa striking force ya hatari kwa Yanga SC kawa hawatajipanga vyema tokea nafasi ya kiungo na walinzi wa kati . Ikumbukwe Azam FC mpaka sasa wamecheza michezo saba katika ligi bila kupoteza.
Morris na Yakubu bado ni walinzi imara wa kati kwa Azam FC ambao leo nadhani mwalimu anaweza kuwaanzisha wakisaidiwa na Kapombe kulia na Kangwa au Gadiel kushoto .
Mechi mbili alizopangwa Kapombe timu ya taifa hakuwa vyema sana lakini bado alicheza vizuri . Bado Azam FC wana kiraka Erasto Nyoni ambaye anaweza kucheza nafasi hiyo.
Yanga SC
Tayari kocha msaidizi wa mabingwa hawa watetezi Juma Mwambusi ametanabaisha wao kama benchi la ufundi toka watoke Zambia kwenye mchezo wa klabu bingwa Afrika dhidi ya Zanaco , wamekuwa wakilishughulikia vyema eneo la kiungo cha chini na safu ya ushambuliaji pia kuwajenga stamina wachezaji wao kupambana dakika zote 90 wakiwa katika nguvu ile ile na kusimama vyema katika kasi na tempo ya mchezo .
Lwandamina amekuwa hatabiriki sana katika upangaji wake wa kikosi hivyo ni ngumu kumsoma mechi kama ya leo atakuja na approach gani na akiwatumia wachezaji gani .
- Kisaikolojia
Yanga SC wanaingia katika mchezo huu wakiwa na msongo wa mawazo pande mbili. Kwanza kabisa ni uhakika wao wa kutetea kombe lao kutokana na kasi ya mahasimu wao Simba SC kulitaka kombe wakiwa kileleni na alama 55 tofauti ya alama mbili na wao wakiwa nafasi ya pili na alama 53. Hii inaweza kuwapa hamasa kusaka ushindi leo au kuwafanya kucheza kwa tahadhari kubwa na kujikuta wakiangukia kwenye defensive patterns kwa asilimia kubwa hali ambayo inaweza kuwapa sare au kufungwa.
Msongo wa pili ni matokeo ya Zanzibar kati yao na wapinzani wao leo . Kwa Legacy ya Yanga SC bara na visiwani kufungwa goli nne! ni fedheha kubwa . Hii inawafanya kuingia uwanjani kwa tension ili lisiwatokee tena . Tension hii kimbinu na kiufundi inaweza kuwasaidia au kuwaangamiza . Wakitaharuki Azam FC wanaweza kuwatoa mchezoni mapema mathalani wakifanikiwa kupata goli la mapema au wakitulia kwenye boxes zote na kila mchezaji akiukumbuka mchezo wa Zanzibar kwa uchungu ili kulipiza kisasi , itakuwa faida kwao .
Tukikiangalia kikosi cha Yanga SC , ni dhahiri watamkosa Amisi Tambwe ambaye bado hajawa fit baada ya majeraha ya muda mrefu . Ngoma nae ameanza mazoezi hivi karibu kitu ambacho hakitupi asilimia 100 mwalimu kumtumia leo.
Majeruhi haya yatamlazimu Lwandamina kuipanga timu yake kama alivyofanya Lusaka Zambia . Chirwa akisimama mshambuliaji wa kati , Niyonzima namba mbili , kulia Msuva na kushoto Emanuel Martini au Deusi Kaseke.
Azam wapo bold sana eneo la kiungo hivyo GL sioni kama ataepuka kuwaanzisha Justine Zulu na Thabani Kamusoko ili kuleta ukinzani kwa Himidi Mao , Sure boy na Frank Domayo.
Kama Azam FC wakija na mfumo wao wa 4-3-3 wakiwa na faida ya kutumia viungo washambuliaji wawili ; Mahundi na Abubakari Salumu, Lwandamina inampasa kuanza na viungo wenye uwezo wa kucheza double pivot si chini ya wawili ili kuivunja nguvu ya viungo wa Azam kujenga mashambulizi pia kuwashambulia kupitia kati ( pressing ).
Lwandamina kuna uwezekano mkubwa kuanza na patterns za 4-2-3-1 . Zulu na Kamusoko wakisimama kati , Msuva, Kaseke/Martin na Haruna Niyonzima wakiwa juu yao na Obrey Chirwa akisimama mbele endapo Ngoma hataweza kuanza kabisa.
Kasi muda wote , kutumia nafasi watakazo zitengeneza na uwezo wa mwalimu kubadili mchezo kwa subs za kueleweka kwa wakati , kunaweza kuipa ushindi Yanga kwenye mechi hii.
Matarajio ya kushinda mchezo wa mtoana na MC Alger , nadhani umelifanya benchi la ufundi la Yanga SC kujiandaa na Azam FC katika viwango vya kuwakabili waarabu hao katika shirikisho kutokana na ratiba kukaribiana sana . Kama ndivyo basi Lwandamina anaweza kuondoka na hesabu sahihi jioni ya leo.
Asanteni.


Post a Comment