Nimekuwa nikimfatilia kwa karibu sana Adenor Leonardo Bacchi al maarufu kama Tite kocha mkuu wa timu ya taifa ya Brazil. Namfatilia kutaka kujua nini hasa kikubwa anakifanya na kikosi hicho ambacho kimemfanya katika miezi tisa! tu aandike historia kubwa ikiwemo; kuwa nchi ya kwanza kufuzu kwa fainali za kombe la dunia msimu huu.
Tite mkongwe huyu aliyevuma na timu ya Corithians, ukimchunguza sana utaelewa mambo mengi ambayo yanamsaidia kukiongoza kikosi kizito zaidi cha soka duniani bila mzingo wa mawazo. Kupata fursa kuiongoza selecao si jambo dogo . Kikosi chenye rekodi ya kubeba kombe la dunia mara tano na kikiwa na wapenzi katika kila pembe ya ulimwengu huu.
Tite alikabidhiwa timu juni 20, 2016 . Alikabidhiwa timu toka kwa Nduga aliyetimuliwa baada ya miamba hiyo ya soka duniani kuonekana wapo hoi bin taabani kupambana kimataifa.
Tite alikabidhiwa timu ikiwa nafasi ya sita! katika msimamo wa kundi la CONMEBOL katika harakati za kufuzu kwa michuano ya kombe la dunia mwaka 2018 nchini Urusi. Nafasi ambayo ilikuwa inatishia wao kuipata fursa ya kuiwakilisha nchi katika michuano hiyo mikubwa zaidi duniani pia hata kukosa fursa ya kucheza Intercontinental play-offs kwa ajili ya kuisaka nafasi hiyo. Hapo utaelewa ni jinsi gani Brazil ilikuwa inazama katika fahari ya soka duniani. Dunga alikuwa amewatia simanzi wapenzi wa Brazil na hatari ya kuporomoka zaidi ilionekana. Tite alipewa timu kama mkombozi wa kuokoa jahazi hili lililokuwa likizama.
Ni miezi tisa sasa imepita . Miezi ambayo Tite amegeuka ' masihi ' wa soka la Brazil kwa kuwakomboa katika anguko ambalo lilikuwa likiwanyemelea. Ndani ya miezi hiyo tisa , ameshinda mechi nane mfululizo . Mechi ambazo zimeipa Brazil ubingwa wa Olympic kwa mara ya kwanza na kuwafanya kuwa wa kwanza kufuzu michuano ya kombe la dunia ambayo hapo awali walionekana kuipungia mkono wa kwaheri.
Nini amekibadirisha Tite kwa Brazil?
Kwanza kabisa kocha huyu mzawa aligundua tatizo kubwa lililomkabili Nduga si uwezo wake mbaya kimbinu na kiufundi kuifundisha timu hii . Mara kadhaa Tite akihojiwa na vyombo vya habari kuangazia uwezo wa mwalimu aliyemtangulia , Tite huwa na maneno machache tu " namuheshimu Nduga ni mwalimu mzuri na ameifanyia makubwa nchi hii akiwa mchezaji wa kikosi hiki pia akiwa kicha .." ndio maneno ya hekima ya Tite kwa mtangulizi wake.
Tite aligundua kikosi kimekosa umoja, upendo na ushirikiano miongoni mwa wachezaji. Neymar Jr alionekana kama mungu mtu kwenye kikosi na kuondoa morali ya wachezaji wengine kuitumikia nchi yao . Mapenzi makubwa ya Nduga kwa baadhi ya wachezaji maarufu ndani ya kikosi yaliwafanya wengine kukosa saikolojia sahihi kuitumikia timu hiyo.
Ukitazama katika mechi nane alizoziongoza Tite na Selicao upande wa manahodha utaelewa nini na maanisha. Kazi kubwa ya kwanza ya Tite ilikuwa kurudisha umoja kitimu kabla ya kuanza kuleta chagizo kimbinu na kiufundi . Katika hizo mechi nane, Brazil imeongozwa na manahodha sita tofauti na kuondoa ile hali ya kukariri kitambaa cha unahodha ni cha Neymar Jr .
Miranda, Dan Alves, Neymar Jr , Fernandinho , Felipe Luis na Renato Augusto hawa ndio kwa nyakati tofauti wamekivaa kitambaa cha unahodha . Hivi ni nani asiyetamani heshima ya kuvaa kitambaa cha unahodha cha timu yake ya taifa? . Kuna raha yake bwana . Mbinu hii ya kuwapa wachezaji mbalimbali kitambaa cha unahodha ndani ya timu hiyo , kimeweza kurudisha umoja kitimu na kuwafanya wachezaji wote kucheza kwa moyo.
Kimbinu na kiufundi..
Tite amefanikiwa kuivunja rekodi ya Brazil ya mwaka 1970 kwa kushinda mechi sita mfululizo kuelekea michuano ya kombe la dunia iliyofanyika nchini Chile kwa yeye kushinda mechi nane mfululizo. Wakati huo Brazil walikuwa wakitumia mifumo miwili ya 4-3-3 na chagizo lao la " samba " pia 3-4-3 . Tite hajatoka mbali sana na mstari wa utamaduni wa soka la Brazil , soka linalotumia idadi kubwa ya viungo na kusimamia kwenye mifumo mipana ( wide formations). Mifumo inayokupa uwiano sawa wa wachezaji katika kushambulia na kujilinda.
Tite anatumia 4-3-3 na 4-1-4-1. Aliposhinda kombe la Olympic, wachambuzi wa soka walimuuliza kwanini anapendelea mifumo hiyo ambayo imezoeleka sana katika kikosi cha Brazil na kuacha baadhi ya mifumo ambayo nchi za ulaya wanaitumia kwa sasa kama 4-2-3-1 ? Tite alijibu , tatizo sio mifumo kuzoeleka bali uwezo wa kuitumia na kupata ushindi . Aliongeza kwa kusema soka si mchezo wa kificho ila inakuhitaji kuwaandaa kwanza wachezaji kisaikolojia kabla hujaingiza kile unachokiamini ili wanapokwenda uwanjani wakisimamie kwa kuongozwa na passion halisi toka moyoni.
" As I see it, the best way I can contribute is by applying the principles that have guided my life and career up to this point: transparency, democratisation, excellence and modernity."
"I'm of the school of thought that it is all about pass and move, give and go, playing in triangles, interplay and creativity in the final third. I don't mind my team being less physically strong in exchange for more mobility and nimble, swift transitions."
Ukisoma vyema katika nukuu hizo hapo juu utamuelewa ni mwalimu wa aina gani . Ni mwalimu ambaye anawekeza zaidi katika saikolojia na mbinu kitu ambacho kinaifanya timu yake kuwa tishio.
Huyo ndio Tite mchawi wa soka la Brazil kwa sasa ambaye ameirudisha Brazil kwenye headlines za soka ulimwenguni .
Imeandaliwa na Samuel Samuel
30. 03. 2017


Post a Comment