Kwa miaka mingi toka Afrika kwa ujumla wake kupata uhuru wa bendera na kuanza kujikita katika soka la ushindani , mafanikio makubwa kisoka yamefikiwa na timu za vijana kuliko timu za wakubwa .
Nigeria mwaka 1996 ilifanya vyema na kikosi chake cha U23 katika michuano ya Olympic kwa kuibuka na medali ya dhahabu ikiwafumua vigogo wa soka duniani Brazil na Argentina.
Kikosi cha U17 cha timu ya taifa ya Ghana al maarufu kama Starlets michuano ya kombe la dunia mwaka 1991 waliibika mabingwa pia 1995 pia wakiingia hatua ya fainali 1993 na 1997 .
Mwaka 1999 hao hao Ghana walitoa mfungaji bora wa dunia Ishmael Addo.
Hii ni baadhi ya mifano tu ya mafanikio ya timu za vijana za Afrika na wachezaji husika lakini tukiangalia timu za wakubwa bado tuna rekodi ya Cameroon tu kuingia robo fainali ya michuano ya kombe la dunia mwaka 1990 na kufungwa na England katika hatua hiyo hatua ambayo pia ilifikiwa na Senegal 2002.
Kuna sababu nyingi sana za timu za vijana kufanikiwa kuliko timu za wakubwa.
Mfumo wa soka
Mfumo wa soka la Afrika ni ngumu sana kuendeleza vipaji vya wachezaji chipukizi au vijana wadogo ambao wanaibukia vyema katika fani hiyo . Utakuta nguvu kubwa inafanyika kupata timu za chini ya umri wa miaka 17, 18, 19 na 20 lakini baada ya mashindano mbalimbali vijana hutelekezwa na inabaki juhudi binafsi kufanikiwa kwa mchezaji husika.
Wenzetu wana utamaduni mzuri wa kulea vipaji kwenye akademi zao mathalani kuingia mikataba na vijana hao wakiwa bado wadogo kitu kinachowafanya kusimamia maendeleo yao na mwisho wa siku kupata timu bora za wakubwa kupitia vijana ambao wamekuzwa vyema katika njia sahihi za soka .
Umasikini
Bara la Afrika limegubikwa na umasikini mkubwa katika kila sekta . Soka ni mchezo ambao unahitaji uwekezaji mkubwa kiuchumi ili kufanikisha maendeleo yake . Vijana wengi wa Afrika wanatoka katika familia masikini sana hivyo hushindwa kumudu gharama mbalimbali za kujihudumia kisoka ili wafike mbali . Mfano kukosa vifaa vya michezo , kula vizuri pia vilabu na mashirikisho mengi ya soka kukosa bajeti stahiki kulea vipaji hivi mwisho wa siku wanajiingiza katika makundi ya uovu kama ulaji wa madawa ya kulevya , kuingia katika ajira za mapema kukidhi mahitaji muhimu ya maisha kama chakula na malazi .
Katika umasikini pia vijana wengi wanakuwa na mentality ya kulikimbia bara la Afrika na kutafuta maisha mazuri Ulaya na mashariki ya mbali kitu ambacho kinatufanya kukosa mwendelezo wao sahihi kisoka au wengine kubadili uraia na kutumikia mataifa ya huko.
Sera na itikadi za serikali zetu
Serikali nyingi za Afrika mchezo wa soka wanauchukulia kama burudani tu na chanzo cha kudumisha amani na umoja wa kitaifa lakini sio ajira rasmi au mfumo mbadala wa kutunisha mifuko yao ya kiuchumi na kwa wachezaji binafsi . Mara kadhaa tumeshuhudia serikali nyingi zikiondoa mchezo huu mashuleni mfano hapa Tanzania kitu ambacho kinakata mizizi ya ukuaji mzuri wa soka la wakubwa. Wenzetu wanawekeza zaidi kwenye soka la vijana pia wanatambua soka kama ajira rasmi kwa nyanja mbalimbali na serikali zao zinakusanya kodi nzuri kupitia mishahara, mauzo ya jezi , mikataba na matangazo ya mipira kwa kiasi kikubwa tu.
Migogoro
Bara la Afrika limegubikwa na migogoro ya kila aina mfano vita vya wenyewe kwa wenyewe , makundi ya ugaidi na vita vya taifa moja juu ya lingine . Popote pale ambapo hakuna amani na utulivu daima hakuna maendeleo. Maendeleo waliyonayo DRC katika soka sasa huenda yangekuwa maradufu lakini hakuna utulivu kitu ambacho kinafanya mchezo wa soka katika nchi hiyo kuchezwa sehemu baadhi tu na kuondoa fursa kwa lundo la vijana wenye vipaji vikubwa kuucheza mchezo huo kwa mafanikio na huenda wangelipaka rangi mpya soka la Afrika ngazi ya kimataifa. Migogoro hii pia inafanya timu , mashirikisho na serikali kukosa fedha za kuwekeza katika soka na mwisho wa siku kuendelea kulitia kilema soka letu.
Rushwa na Ubadhirifu
Viongozi wengi wa soka Afrika ni wala rushwa wakubwa na wabadhirifu katika sekta hiyo hali ambayo imeathiri soka la Afrika kwa kiasi kikubwa . Fedha nyingi za maendeleo toka FIFA zinaishia kwenye matumbo na mifuko yao kitu ambacho kinawafanya washindwe kulifanya bara letu kusogea mbele kisoka na kuleta ushindani mzuri na mataifa mengine.
Serikali kuingilia masuala ya soka
Hapa juzi tumeona taifa la Mali likifungiwa na FIFA kushiriki michuano inayoandaliwa na shirika hilo pamoja na washirika wake kwa serikali ya nchi hiyo kuingilia tu masuala ya soka kwa kuyafanyia maamuzi kinyume na taratibu za FIFA . Hili ni tatizo pia ambalo linadumaza ukuaji wa soka letu na kukosa timu imara za taifa kushindana na wenzetu.
Kukosa uzalendo
Vijana wengi wa kiafrika wakifanikiwa katika ligi kubwa barani ulaya hukosa uzalendo wa kutumikia mataifa yao . Wapo ambao huanzisha migomo kwa malipo kiduchu kutoka katika mashirikisho yao ; tuliliona hili vyema kwa Cameroon michuano ya AFCON mwaka huu . Wenzetu wana fahari kubwa kuchezea timu zao za taifa hata kama ni malipo kiduchu.
Miundo mbinu mibovu
Miundo mbinu ya soka la Afrika kwa kiasi kikubwa ni mibovu na sehemu nyingine hakuna kitu ambacho kinaathiri ukuaji wa soka letu . Hatuna shule nzuri za mpira , viwanja vya mazoezi na vya kuchezea kuongeza passion kubwa ya vijana kucheza mpira kwa mafanikio.
Udanganyifu wa umri
Tumebobea katika hili . Timu zetu nyingi za vijana zinafanya vyema kutokana na udanganyifu wa umri na ndio maana vijana wetu wanashindwa kufika mbali kutokana na kudanganya umri hivyo huwika miaka miwili mitatu basi . Mtazame Christiani Ronaldo kaibuka lini katia soka na mpaka sasa katika umri wa miaka 31 bado ni mwiba mkali.
Ligi dhaifu
Ligi zetu ni dhaifu sana ambazo hazitoi ushindani wa kutosha ili vijana wetu wapitie moto mkali ili hata wakiitwa timu za wataifa waende kutoa upinzani mkali . Ligi nyingi zina timu chache , dhaifu na rushwa michezoni ni kubwa kitu ambacho kinatufanya kucheza katika kiwango duni na mwisho wa siku kupata timu za taifa za wakubwa dhaifu na kuishia kila mwaka kufungwa tu.
Yapo mengi sana lakini leo naishia hapo tukutane tena siku nyingine .
Samuel Samuel
Post a Comment