Na: Ayoub Hinjo
Mzunguko wa dunia katika muhimili wake husababisha vitu vingi kutokea kwa viumbe hai na visivyo hai vilivyomo ndani yake ambavyo huwa na faida au hasara kwa viumbe hivyo.
Bahati ilioje kwa mzunguko huo kutuletea kiumbe hai ambacho hakizungumzwi na wenzake!? Hata vyombo vya habari vimekuwa havimgusi sana labda havutii kurasa za mbele za magazeti ya michezo.
Kikosi cha Simba kimezungukwa na wachezaji wengi waliojaa vipaji na wenye uwezo mkubwa. Sehemu waliyopo kwenye msimamo wa ligi kuu haishangazi hata kidogo.
Ni moja ya utimilifu kamili wa timu kuweza kuzalisha magoli kutoka katika pande au eneo la uwanja kama ilivyo kwa Simba sasa. Yanga ilifanikiwa kuwa katika ukamili huo kwa muda mrefu na kuwafanya kutawala soka la nchini kwa muda kidogo.
Mzunguko na mgawanyo wa magoli yanayofungwa na wachezaji wa Simba kwa asilimia karibu 60 yametokea eneo la katikati ambapo kuna shujaa asiyeimbwa anaitwa Mzamiru Yasini aliyefunga magoli 6.
Uwezekano wa Mzamiru kuongeza magoli mengine ni mkubwa sana sababu ana uwezo wa kunusa harufu ya goli kwenye sanduku la adui kuliko hata washambuliaji wake(Mavugo na Blagnon) ambao wote wawili ukiweka pamoja magoli yao hawamfikii Mzamiru.
Kamusoko kashindwa kuendelea alipoishia msimu ulioipita ambao alifunga magoli 5 mengi kuliko kiungo yoyote wa kati. Lakini tayari msimu huu Mzamiru katupia zaidi ya Kamusoko.
Mtihani mkubwa kwa Mzamiru ni kutuonyesha kuwa anaweza kuwa kama Frank Lampard,Yaya Toure na viungo wengine ambao walikuwa wanafunga magoli mengi licha ya kuwa na washambuliaji wakali kwenye timu zao.
Ndani ya kikosi cha Simba nafasi ya Mzamiru ni ya wazi. Nafasi yake si yakumuumiza kichwa Omog kama akiwa katika kiwango chake cha juu kama ilivyo siku zote. Sababu ni moja ya wachezaji wachache muhimu ambao wanaweza kumudu kucheza katika viwanja tofauti tofauti vya mikoani na wakakupa matokeo.
Mzamiru ni shujaa asiyeimbwa midomoni mwa mashabiki wa Simba na hata wale wa upande wa pili. Ni rahisi kusahaulika sababu hakuja kwa mbwembwe wala si mtu wa kuonekana sana nje ya kazi yake ya uwanjani.
Muda wa kuwa Lampard au Toure bado anao. Uzuri ni kwamba hata yeye mwenyewe haonekani kupenda kuwa katika midomo ya mashabiki licha ya kutajwa katika maongezi yao.
Post a Comment