Na Samuel Samuel
Mabingwa mara 27 wa ligi kuu Tanzania bara leo watakuwa uwanja wa kumbukumbu ya Sheikh Amri Abeid katika mechi ya kirafiki ya kihistoria na timu ya jiji la Arusha , timu kongwe na kipenzi cha wakazi wa Arusha AFC.
Baada ya kufanya vizuri kwenye kombe la ligi na kufanikiwa kunyakua ubingwa wa ligi hiyo msimu huu , Yanga SC walipata mwaliko maalumu toka kwa wakali hao wa zamani katika jiji la Arusha wakitamba mwanzoni mwa miaka ya 2000 katika uga wa ligi kuu Tanzania bara . Kuthamini mchango wa wakazi wa Arusha katika soka la nchi hii hususani wapenzi na mashabiki wa Yanga , uongozi wa Yanga uliridhia ombi hilo na jioni ya leo wakazi wa mji huo watashuhudia mtanange huo.
Unakuwa mtange wa kihistoria kwakuwa Yanga SC haijawahi kucheza mechi ya kirafiki katika jiji la Arusha na mechi ya mwisho kwa wanajangwani hao katika uwanja wa Sheikh Amri Abeid , ilikuwa msimu wa 2013-14 dhidi ya Oljoro JKT na Yanga kuibuka washindi kwa goli 2-1.
Kuthamini mwaliko huo Yanga ipo hapa jijini Arusha na kikosi chake kamili ukiondoa baadhi ya wachezaji ambao wapo katika timu zao za taifa. Saimoni Msuva , Beno Kakolanya na Mwinyi Haji walioko katika kambi ya taifa Stars . Mwingine ni Thabani Kamusoko aliyeitwa katika timu yake ya taifa ya Zimbabwe.
AFC wakiwa katika mikakati maalumu ya kuunda kikosi chao kinachojumuisha damu changa na baadhi ya wakongwe waliovuma katika timu mbalimbali za ligi daraja la kwanza msimu uliopita , wametamba leo kuwapa upinzani mkali mabingwa hao wa ligi kuu Tanzania.
AFC ni zaidi ya wiki mbili sasa wamekaa kambini wakijianda kwa ajili ya mchezo wa leo . Ni mechi ambayo wao wanaamini itawarudisha vyema katika ramani ya soka nchini baada ya kukaa kimya kwa muda mrefu . Uongozi wa klabu hiyo jana wakifanya mahojiano na Yanga TV Online walisema sehemu ya mapato ya mchezo wa leo watayatumia kwa ajili ya usajili na tayari wafadhili mbalimbali wamejitokeza kuipa sapoti timu hiyo yenye idadi kubwa ya mashabiki Arusha ili waweze kujipanga vyema.
Kocha msaidizi wa Yanga SC ndugu Juma Mwambusi aliyeko na timu Arusha baada ya kocha mkuu George Lwandamina kubaki Dar es salaam kutokana na kuumwa , amesema yupo tayari kukabiliana na upinzani mkali toka kwa vijana wa AFC .
" mechi kama hizi inakupasa kuchukua tahadhari kubwa . Vijana huwa wanakamia na kucheza kwa nguvu muda wote ili kushinda dhidi ya timu kubwa pia kujiweka vyema sokoni . Tunauchukulia umuhimu mkubwa mchezo huu ukiwa ni sehemu ya maandalizi ya yetu kabla ya michuano ya SportPesa inayoanza juni 5.
Mechi ya wababe hawa inaanza saa 10:00 jioni .
Post a Comment